Burudani

Mkali wa Jiko kuondoka na donge nono

DAR ES SALAAM: MSHINDI wa shindano la Mkali wa Jiko msimu wa sita anatarajiwa kuondoka na zawadi ya Shilingi milioni tano pamoja na kusomeshwa Chuo cha Taifa cha Utalii, sambamba na fursa mbalimbali za ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mratibu wa shindano hilo, Zainabu Issa, amesema msimu wa sita wa mashindano hayo unalenga kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao katika sanaa ya upishi na kupata fursa za kujifunza zaidi kuhusu sekta ya utalii na huduma za chakula.

Amesema chakula ni sehemu muhimu ya utambulisho wa mtu na taifa, huku akieleza kuwa upishi ni sanaa inayohitaji ubunifu, umakini na ujuzi wa kuandaa vipimo sahihi vya mapishi.

“Tunawaalika watu mbalimbali kushiriki katika shindano hili na kuonyesha ufundi wao wa kupika. Upishi ni sanaa inayotegemea ubunifu na uwezo wa kuandaa chakula kwa ustadi mkubwa,” amesema Zainabu.

Aidha, amesema washiriki 20 watachaguliwa kushiriki kwenye programu hiyo itakayodumu kwa miezi minne hadi kufikia kilele cha mashindano kitakachofanyika Oktoba mwaka huu.
Usaili wa washiriki unatarajiwa kufanyika Juni 20, 2026, katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.

Washiriki watakaofanikiwa kupita hatua ya usaili wametakiwa kuzingatia maelekezo ya majaji ili kuongeza nafasi zao za kufanya vizuri katika mashindano hayo.

“Ni burudani, lakini pia ni sehemu ya kuonyesha kipaji chako na ufundi wako wa upishi,” ameongeza.

Akitaja vigezo vya ushiriki, Zainabu amesema mshiriki anatakiwa kuwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, huku walio kwenye ndoa wakitakiwa kupata ridhaa kutoka kwa wenza wao kabla ya kushiriki.

Kwa upande wake, Mkufuzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Ong’oso Mwita, amesema chuo hicho kiko tayari kuwapa nafasi ya masomo washindi wa mashindano hayo ili kuwawezesha kukuza taaluma zao katika sekta ya utalii na huduma za chakula.

“Tutawasomesha washiriki watakaoshinda katika shindano hili kwa kuwapatia nafasi ya masomo katika chuo chetu,” amesema Mwita.

Related Articles

Back to top button