Ligi Daraja La Kwanza

Stars kujiweka mguu sawa kwa AFCON 2027

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema michezo ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda na Rwanda ni sehemu ya maandalizi ya timu katika kujiweka tayari kwa mashindano mbalimbali yajayo ikiwemo Afcon.

Akizungumza Dar es Salaam Ndimbo amesema mchezo wa kwanza utachezwa Juni 5 dhidi ya Uganda huku mchezo wa pili ukitarajiwa kuchezwa Juni 9 dhidi ya Rwanda.

Amesema benchi la ufundi chini ya Kocha Gamondi linaendelea kufanya tathmini ya kikosi kwa kuangalia uwezo wa wachezaji wanaoitwa mara kwa mara pamoja na wengine wapya wanaopewa nafasi ya kuonesha uwezo wao.

“Kocha anaendelea kufanya tathmini ya kikosi kulingana na mahitaji ya timu na mashindano yaliyopo mbele yetu,” amesema Ndimbo.

Amesema kuwa baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipata nafasi mara kwa mara kutokana na viwango vyao huku wengine wakipewa nafasi kwa lengo la kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

Ndimbo amesema michezo hiyo itatoa nafasi kwa benchi la ufundi kuona maeneo yanayohitaji maboresho huku lengo kubwa likiwa kujenga timu imara na yenye ushindani mkubwa.

Leo taifa Stars wataingia kambini na kesho wataelekea Morocco kujiandaa na michezo hiyo miwili.

Related Articles

Back to top button