Kwingineko

Madrid njia nyeupe kwa Konate

Real Madrid yapata nguvu kumsajili beki wa Liverpool

MADRID: REAL Madrid imepata nguvu mpya katika harakati za kumsajili beki wa Liverpool, Ibrahima Konate, wakati klabu hiyo ikisaka mbadala wa David Alaba anayetarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania, Konate alikuwa mmoja wa malengo makubwa ya Real Madrid tangu msimu uliopita huku mabosi wa klabu hiyo wakivutiwa na uwezo wake mkubwa katika safu ya ulinzi.

Awali, mipango ya Real Madrid ilikuwa ni kumsajili beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa bure baada ya mkataba wake na Liverpool kumalizika, jambo ambalo limekuwa sehemu ya mkakati wao wa usajili katika miaka ya karibuni.

Katika misimu ya hivi karibuni, Real Madrid imefanikiwa kuwanasa mastaa kadhaa bila ada ya usajili akiwemo Antonio Rudiger, Kylian Mbappe pamoja na Trent Alexander-Arnold.

Sasa Konate ameibuka tena kwenye rada za mabingwa hao wa Hispania huku taarifa zikidai kuwa kuna uwezekano mkubwa wa dili hilo kufanikishwa katika dirisha lijalo la usajili.

Real Madrid inaendelea kutafuta maboresho katika safu ya ulinzi baada ya kukumbwa na changamoto za majeraha pamoja na mabadiliko ya kikosi kuelekea msimu mpya.

Konate amekuwa mmoja wa mabeki muhimu wa Liverpool kutokana na uwezo wake wa kuzuia mashambulizi, nguvu katika mipira ya juu pamoja na utulivu akiwa ndani ya uwanja.

Related Articles

Back to top button