Kwingineko

Messi yuko ‘fiti’ kwa Kombe la Dunia

BUENOS AIRES: NAHODHA wa Argentina, Lionel Messi anatarajiwa kucheza Kombe la Dunia la sita baada ya kutajwa kwenye kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia 2026.

Messi, ambaye atakuwa na miaka 39 wakati wa mashindano hayo, ameendelea kuandika historia akiwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani baada ya kuiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

Nyota huyo wa Inter Miami tayari anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi za Kombe la Dunia akiwa amecheza michezo 26, huku akitarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji wachache kuwahi kushiriki matoleo sita ya mashindano hayo makubwa duniani.

Kocha Lionel Scaloni alimtaja Messi katika kikosi cha wachezaji 26 kitakachoshiriki michuano hiyo itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Katika kikosi hicho pia wamo kipa Emiliano Martinez wa Aston Villa, beki Lisandro Martinez wa Manchester United pamoja na Cristian Romero wa Tottenham Hotspur.

Wachezaji wengine waliopo kwenye kikosi hicho ni Alexis Mac Allister wa Liverpool, Enzo Fernandez wa Chelsea, Julian Alvarez wa Atletico Madrid pamoja na Lautaro Martinez wa Inter Milan.
Argentina inaanza kampeni zake za Kombe la Dunia kwa mchezo dhidi ya Algeria kabla ya kucheza dhidi ya Austria na Jordan katika hatua ya makundi.

Messi ambaye hivi karibuni alipata changamoto ndogo ya uchovu wa misuli akiwa na Inter Miami, anatarajiwa kuendelea kuwa tegemeo kubwa la Argentina katika harakati za kutetea ubingwa wao wa dunia.

Mbali na majina makubwa yaliyopo kikosini, baadhi ya wachezaji maarufu wameachwa akiwemo Paulo Dybala pamoja na kinda wa Real Madrid, Franco Mastantuono.

Related Articles

Back to top button