Nyumbani

Wawili Serengeti Boys waula Stars

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amewaongeza wachezaji wawili wa Serengeti Boys katika kikosi cha timu ya taifa kuelekea michezo miwili ya kirafiki ya kalenda ya FIFA itakayochezwa nchini Morocco.

Wachezaji walioitwa ni Luqman Mbalasalu na Kassim Juma ambao kwa sasa wapo na kikosi cha Serengeti Boys kinachoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF Clifford Ndimbo Leo, nyota hao watajiunga rasmi na Taifa Stars mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali wa AFCON U-17 kati ya Tanzania na Senegal utakaochezwa Juni 2 nchini Morocco.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Uganda Juni 5 kabla ya kuvaana na Rwanda Juni 9 mjini Marrakech.

Gamondi ameonesha kuvutiwa na kiwango kinachooneshwa na vijana hao katika michuano ya AFCON U-17, ambapo wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Serengeti Boys kutinga hatua ya fainali.

Hatua ya kuwaita vijana hao imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa benchi la ufundi kuendelea kujenga kikosi chenye ushindani na kutoa nafasi kwa vipaji vinavyoibukia kufanya kazi pamoja na wachezaji wakubwa wa timu ya taifa.

Serengeti Boys imeendelea kuonesha kiwango bora katika michuano hiyo inayoendelea nchini Morocco na kuwavutia wadau wengi wa soka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, wachezaji wengine walioitwa katika kikosi hicho wanatarajiwa kuripoti kambini leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michezo hiyo.

Related Articles

Back to top button