Kwingineko

Barcelona yapania kumng’oa Alvarez ndani Atletico

BARCELONA: KLABU ya Barcelona inadaiwa kuandaa ofa ya Euro milioni 90 kwa ajili ya kumng’oa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, baada ya kufanya mazungumzo na mawakala wa nyota huyo wa Argentina.

Alvarez mwenye umri wa miaka 26 ametajwa kuwa chaguo kuu la Barcelona kuchukua nafasi ya mshambuliaji mkongwe Robert Lewandowski huku taarifa zikieleza kuwa nyota huyo ameonyesha nia ya kujiunga na miamba hiyo ya Catalonia.

Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Deco, alikutana kwa zaidi ya saa nne na wakala wa Alvarez, Fernando Hidalgo, kujadili uwezekano wa kukamilisha usajili huo kabla ya Kombe la Dunia.

Hata hivyo, Atletico Madrid wanaelezwa kutokuwa tayari kumuachia kirahisi mshambuliaji huyo huku wakihitaji dau la zaidi ya Euro milioni 150 ili kukubali kufanya biashara hiyo.

Mbali na Barcelona, vilabu vya Paris Saint-Germain na Arsenal pia vinatajwa kuwania saini ya mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na msimu mzuri tangu ajiunge na Atletico.

Barcelona wanaonekana kuwa na harakati kubwa katika dirisha hili la usajili baada ya taarifa za kukamilisha makubaliano ya kumsajili Anthony Gordon kutoka Newcastle United.

Pamoja na mipango hiyo, wachambuzi wa soka Hispania wanahoji uwezo wa kifedha wa Barcelona kukamilisha usajili huo mkubwa bila kuuza baadhi ya wachezaji wake kutokana na masharti ya matumizi ya fedha yaliyowekwa La Liga.

Alvarez anaonekana kuwa mmoja wa washambuliaji wanaotafutwa zaidi Ulaya kwa sasa kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao, kucheza kwa nguvu na kusaidia timu katika maeneo mbalimbali ya ushambuliaji.

Related Articles

Back to top button