DAR ES SALAAM: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kazi ya mshambuliaji wao Kibu Denis ni kulegeza njia za wapinzani ili kurahisisha kazi kwa washambuliaji wa timu hiyo.
Amesema suala la kufunga msimu huu sio jukumu lake bali wamewapa watu wengine akiwemo Steven Mukwala, Leonel Ateba na kiungo Charles Ahoua.
“Ni muhimu kutambua kila mchezaji ana thamani yake, kuna kazi ambayo tunataka mchezaji afanye, kuna mjadala mkubwa kwanini Kibu hajafunga mwaka mzima!
Ni kweli hajafunga ,Simba mbona hatumdai bao, ushamuona mwanasimba anamdai Kibu, kazi yake ya msingi sio kufunga ni kuhakikisha analegeza njia kwa wapinzani kule mbele, waliopewa jukumu la kufunga wanafanya kazi yao,” amesema Ahmed na kuongeza kuwa
Kila mechi anapangwa kwa sababu kazi yake anaifanya ipasavyo , ingekuwa benchi la ufundi linaloongozwa na Fadlu Davids linamtaka afunge asingecheza lakini Kibu panga pangua ndani ya Simba kwa sababu anatekeleza majukumu yake kwa asilimia kubwa.