Kocha Ken Gold aanika sababu za kubwaga manyanga
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Ken Gold FC, Fikir Elias ameweka wazi kuwa amejitathimini na kuamua kuachia ngazi kuinoa timu hiyo kwa kuwa hawezi kufikia malengo waliyojiwekea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25.
Jumatatu Septemba 16, uongozi wa Ken Gold FC ulitoa taarifa kuwa Kocha Fikir na Msaidizi wake, Luhanga Makunja wameomba kuondoka ndani ya timu hiyo.
Kocha huyo amesema ameamua kukaa pembeni na kupisha watu wengine kwenda kuchukuwa nafasi ya kuinoa timu hiyo kufikia malengo yanayotarajiwa na mashabiki na viongozi wa timu hiyo ikiwemo kuleta ushindani kwenye ligi hiyo.
“Ni mechi tatu zote tumepoteza, nimejitathimini mwenyewe na kuona bora nikae pembeni kwa kupisha makocha wengine waje kuendelea hapa nilipoishia” amesema Kocha huyo.
Ameongeza kuwa timu ina mapungufu madogo ikiwemo changamoto ya kucheza kwa presha kutafuta matokeo katika michezo mitatu ambayo wameshacheza na kupoteza yote.
Ken Gold ilipoteza nyumbani kwa kichapo cha mabao 3-1 na Singida Black Stars, 2-1 kutoka kwa wenyeji wao Fountain Gate FC na 1-0 dhidi ya KMC FC.
Baada ya Fikir kuondoka timu hiyo imerejeshwa mikononi mwa kocha Jumanne Charles aliyeipandisha ligi kuu msimu wa 2024/25.