Yanga yamkwamisha Kamwe kuoa

DAR ES SALAAM: Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema anatumia muda mwingi kuwahudumia mashabiki wa timu hiyo kuliko kujali mambo yake binafsi kwani ana mapenzi ya dhati kwao.
Akizungumza kuhusu jinsi anavyoweza kumudu maisha yake binafsi na maisha ya kazi ameeleza kuwa kwasasa haoni ugumu wowote licha ya majukumu mazito aliyonayo akitamba kuwa amechagua kuwatumikia mashabiki wa Yanga.
Kuhusu mahusiano Kamwe amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja hayupo kwenye mahusiano kwani muda mwingi anautumia kufanya kazi anayoipenda ya kuwapa furaha mashabiki wa Yanga huku akisisitiza kuwa muda ukifika atafanya maamuzi.
Ameongeza kuwa muda mwingi anapokea simu za wanachama wa klabu hiyo na kuwapa muda wa kusikiliza maoni yao kuhusu mambo mbalimbali klabuni hapo jambo amabalo anaamini angekuwa na mahusiano lisingewezekana.
“Nitaoa lakini kwa sasa nipo nipo kwanza, nipo Single mwaka na nusu sasa nipo ‘bize’ na mashabiki wangu wa Yanga nawahudumia wao kwa kupokea simu zao na kusikiliza maoni yao kwa sasa ni ngumu kupata muda wa kufanya hivyo” amesema Kamwe.
Katika siku za hivi karibuni Kamwe amekuwa kivutio kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kuja na miradi mbalimbali ya kibunifu ya kuwaunganisha mashabiki wa timu hyo na sasa ameingia katika mwaka wa tatu wa utumishi wake ndani ya kikosi hicho.