Waamuzi, Majaji 26 wamefaulu IBA

WAAMUZI na Majaji 26 kutoka Tanzania wamefaulu mafunzo ya Kimataifa ya Waamuzi na Majaji yaliyotolewa na Chama cha Ngumi cha Kimataifa (IBA) ngazi ya Nyota moja, yaliyofanyika katika Chuo cha taaluma ya Polisi Dar es salaam mwezi uliopita.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na wakufunzi Sadie Duffy kutoka Jamhuri ya Ireland ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Waamuzi na Majaji wa IBA na Godavarisingh Rajcoomar kutoka Mauritius ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Waamuzi na Majaji wa Shirikisho la Ngumi Afrika (AFBC) na yalishirikisha jumla ya Waamuzi na Majaji 39 kutoka Tanzania (29), Kenya (8), Uganda (1) na Namibia (1).
Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo amethibitisha kupokea taarifa ya IBA jana kuhusu waliofaulu mitihani baada ya mafunzo hao ya kimataifa.
“Ni historia kubwa katika utawala wa Shirikisho chini ya Uongozi wa Rais Lukelo Willilo kuweza kuwaendeleza Waamuzi na Majaji kwa idadi kubwa kupata mafunzo na vyeti vya Kimataifa,
kauli yangu ya siku zote ni ile ile, tunaendelea kutekeleza kwa vitendo ndoto yangu ni kuona waamuzi wetu wakisimamia mashindano makubwa Afrika na Duniani,”amesema.
Sasa Tanzania ina jumla waamuzi na majaji 27 wa Kimataifa wenye hadhi ya Nyota moja ya Dunia wakitokea Uraiani, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa TPBRC, Polisi, Magereza, JKT na JWTZ.