Mwakinyo arusha jiwe kuhusu maslahi

DAR ES SALAAM: BONDIA wa ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo amerusha jiwe kwa wadau wa ngumi kwa kusema kuwa kila wanaposimamia maslahi makubwa kwa mabondia wanaonekana makunguru waoga kutaka hela nyingi.
Wakati huo huo, ametoa pole kwa familia ya bondia aliyepoteza maisha hivi karibuni akiwa ulingoni Hassan Mgaya akisema ni mara ya tatu wanazika watu kwa vifo vya aina hiyo.
Mwakinyo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Instagram, amesema “Leo kiasi cha malipo ya sh 60,000 ndio kimekatisha safari ya ndugu yetu…. na wengine wana pigania mpaka magari yaliyotumika. Huu ni ujinga tunapaswa kuwa mifano kwa maslahi ya wengi,”
“Binafsi mimi nasimama na promota wa hilo pambano ya kuwa yeye hana makosa amelipa mabondia kulingana na uwezo wake, wengi wakubwa hawathamini mabondia wadogo,”
Ametoa rai na kusema serikali ingetoa macho kupitia ngumi kuhakikisha kunapatikana wadhamini hata kwa mapambano madogo ya mitaani ili mabondia wadogo wanufaike.
“Hili liwe fundisho kwa mabondia wengine na sasa waachane na ngumi za mkali nani, ukifa haufi na unaowafurahisha unakufa peke yako,”alisema.
Mgaya alipoteza maisha Desemba 29 mwaka jana katika hospitali ya Mwananyamala kufuatia kupigwa kwa TKO na mpinzani wake Paulo Elias katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa Dunia ndogo uliopo Tandale kwa mtogole.