Majiha hatanii nyie
MBEYA: BONDIA wa ngumi za kulipwa Nchini, Fadhili Majiha amefanikiwa kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBC Afrika kwa kumchapa kwa pointi Sabelo Ngebiyana wa Afrika Kusini huku Abeid Zugo akichapwa kwa KO na Mkenya, Albert Kimario.
Katika pambano hilo la Ngumi imenyooka lililofanyika jijini Mbeya kwenye Ukumbi wa New City Pub, Majiha ameshinda kwa ushindi majaji watatu katika pambano hilo la raundi kumi.
Majiha alianza kwa kasi pambano hilo na kumungusha chini Sabelo katika raundi ya kwanza kabla ya kuinuka na kuendelea na pambano hilo lililomalizika bila ya kuwepo kwa KO.
Majiha ameshinda kwa majaji wote watatu kwenye pambano hilo limechezeshwa na Maybin Kante wa Malawi huku jaji wa namba moja wa Tanzania, John Chagu akitoa pointi 99-90 wakati Elton Ndosine wa Malawi huku Erick Khoza wa Afrika Kusini akitoa 98-93.
Baada ya pambano hilo Majiha amesema ameshindwa kuonyesha mchezo mzuri licha ya ushindi alioupata kutokana hali ya hewa wa Mbeya huku akimuomba Spika wa Bunge, DK Tulia Ackson ampelekee zawadi ya mkanda huo kwa kuwa ameshinda akiwa kwenye jimbo lake.
Katika upande mwingine, Abeid Zugo amepoteza pambano kwa KO ya raundi ya nne dhidi ya Albert Kimario ambapo baada ya pambano hilo, Zugo aliwaomba radhi Watanzania huku akidai kuwa amecheza pambano hilo akiwa na majeruhi ya mkono.
Upande wa Idd Pialali amefanikiwa kumchapa kwa pointi Kiaku Ngoy wa DR Congo katika pambano la raundi nane wakati Emmanuel Mwakyembe akimpopoa kwa pointi Gabriel Ochieng wa Kenya.
Mubaraka Denso yeye amefanikiwa kumchapa kwa pointi, George Kandulo wa Malawi huku Kelvin Ngedere akimchapa kwa pointi Yohana Kayuni wakati Mkaveli Mponji akimpiga kwa pointi Erick Muchunguzi huku Emmanuel Amosi akimchapa kwa pointi Nasibu Habibu.