Mastaa

Steve Nyerere: Wasanii wekezeni acheni kuigiza maisha

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amewataka wasanii wa kike kuwekeza katika maendeleo yao badala ya kuingia kwenye ushindani wa maisha ya anasa usioendana na uwezo wao.

Steve alitoa ushauri huo alipokuwa kwenye mazungumzo pamoja na wasanii Shilole na Lulu Diva, baada ya kuulizwa ni ushauri gani anaoweza kuwapa mabinti wanaopata nafasi ya kukubalika na kujijengea jina nchini.

Kabla hajaanza kujibu, Shilole alimgeukia Lulu Diva na kusema kwa utani, “Lulu Diva sikiliza kwa makini, maana wewe tayari umeshaharibikiwa.” Kauli hiyo ilimfanya Lulu Diva kujibu kwa kicheko akisema, “Nimeharibikiwaje? Tuache kuharibiana CV, mambo yangu yanaenda vizuri, utasemaje nimeharibikiwa?”

Akitoa ushauri wake, Steve amesema wasanii wa kike wanapaswa kuepuka kutumia kipato chao katika mambo ya anasa kama ushindani wa mavazi ya gharama, mawigi na nyumba za kifahari ambazo haziendani na uwezo wao wa kifedha.

“Mtoto wa kike ukipata bahati ya kukubalika katika nchi hii, usiwekeze kwenye mawigi, kuvaa wala ushindani wa kupanga nyumba za kifahari wakati uwezo huo huna.

Madhara yake unajikuta unaingia kwenye utegemezi wa watu mbalimbali kwa ajili ya kugharamia maisha yako,” amesema Steve.

Ameongeza kuwa mafanikio yanahitaji nidhamu ya kifedha na utayari wa kupokea ushauri, akisisitiza kuwa mabinti wengi hukosea kwa kuamini kuwa wanajitosheleza huku wakipuuzia ushauri wa watu wenye uzoefu.

“Ukipata nafasi ya kufanya vizuri, ifanyie kazi. Na ukiona unakosea, kubali kushauriwa. Mabinti wengi hawapendi ushauri kwa sababu wanaamini wanajiweza, ilhali wakati mwingine wanafuata tu makelele ya kushangiliwa badala ya kujenga maisha yao ya baadaye,” amesema.

Related Articles

Back to top button