Simba Queens yaifanyia umafia Yanga Princess

DAR ES SALAAM: Simba Queens imedhamiria kuboresha kikosi chake na kwenda kuibomoa Yanga Princess kwa kuchukua nyota watatu kutoka ndani ya timu hiyo ya Wananchi.
Timu hiyo imefanikiwa kumsajili kiungo mkabaji Saiki Mary Atinuke kutoka Nigeria, beki wa kushoto Wingate Kaari (Kenya) na kiungo Precious Christopher ambapo wote wamesaini mkataba wa miaka miwili kutumikia Simba Queens kwa msimu wa 2024/25.
Meneja wa Simba Queens, Seleman Makanya ameiambia Spotileo kuwa usajili wa nyota hao unalenga kutengeneza timu nzuri na bora kwa lengo la kufanya vizuri katika ligi ya ndani na michuano ya kufuzu fainali za Afrika kwa wanawake kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Simba Queens imepangwa kundi B, ambapo timu nyingine ni kama PVP Buyenzi kutoka Burundi, Kawempa Muslim (Uganda) na Fad Djibouti (Djibouti), mashindano hayo yataanza rasmi Agosti 17 hadi Septemba 4, mwaka huu, Mji wa Addis Ababa,nchini Ethiopia.
“Msimu ujao tumedhamiria kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na kimataifa ndio maana tumesajili wachezaji bora na Saiki amekuja kuongeza nguvu kwenye kiungo wa ulinzi na kusaidia kupandisha timu.
Precious na Wincate ni wachezaji wazuri, wamefanya vizuri kwenye timu zao walizotoka na tunatarajia kusaidia timu yetu kwa msimu ujao wa mashindano ,” amesema Seleman.