Ripoti rasmi yaonesha chanzo cha kifo cha Gene Hackman na mkewe

NEW MEXICO: Ripoti rasmi kuhusu vifo vya muigizaji mkongwe Gene Hackman na mkewe, Betsy Hackman, imetolewa, ikieleza kuwa walifariki kwa sababu tofauti za kiafya.
Kwa mujibu wa mchunguzi mkuu wa matibabu wa New Mexico, Heather Jarrell, Hackman alifariki kutokana na shinikizo la damu na ugonjwa wa mishipa ya moyo (atherosclerosis), huku akiwa pia na Alzheimer’s. Mkewe Betsy alikumbwa na ugonjwa adimu wa kupumua, ‘hantavirus pulmonary syndrome,’ unaosababishwa na virusi vinavyopatikana kwenye kinyesi cha panya.
Uchunguzi umeondoa uwezekano wa sumu kuwa chanzo cha vifo hivyo. Inasadikiwa Hackman alifariki Februari 18, huku Betsy akiwa amekufa Februari 11.
Miili yao ilipatikana Februari 26 nyumbani kwao New Mexico. Hackman, aliyekuwa na miaka 95, alipatikana amevalia kikamilifu katika chumba cha kulala, huku mwili wa Betsy (65) ukiwa bafuni karibu na vidonge vilivyotawanyika. Inaaminika kutokana na hali yake ya Alzheimer’s, Hackman hakutambua kuwa mkewe alikuwa tayari amefariki.
Katika nyumba hiyo, mbwa wao mmoja pia alikutwa amekufa, huku wawili wakiwa hai.