Dude: Bongo Dar es Salaam, makubaliano sio rafiki

MWIGIZAJI wa filamu Kulwa Kikumba ‘Dude’ amesema makubaliano ya kimaslahi na televisheni mbalimbali ni sababu inayomfanya kushindwa kuendelea na tamthilia ya Bongo Dar es Salaam.
Baada ya ukimya takribani miaka minne, HabariLEO ilimtafuta Dude kufahamu nini kinachokwamisha tamthilia hiyo kutoonekana na mwelekeo wake kwa sasa.
“Mimi nahitaji pesa kwa ajili ya kuwezesha kutengeneza hivyo vipindi, ila makubaliano yetu yalikuwa mpaka tupate mdhamini, kampuni zingine nimejaribu ila tunashindwa kuelewana,” amesema Dude.
Dude amesema ameanza upya kurekodi tamthilia hiyo na sasa anajipanga kuanza kuzisambaza kutafuta televisheni inayoweza kurusha maudhui yake.
Bongo Dar es Salaam ni tamthilia ya muda mrefu inayofundisha namna Watanzania wanapaswa kuepukana na utapeli, wizi na ujambazi unaofanywa na baadhi ya watu wenye nia ovu miongoni mwa jamii.