Denzel Washington ndani ya Black Panther 3

NEW YORK: MTAYARISHAJI wa filamu, Marvel Nate Moore amesisitiza kuwa ni mapema kwake kusema kama muigizaji nguli Denzel Washington atakuwa miongoni mwa waigizaji katika filamu ya tatu ya ‘Black Panther’.
Nyota huyo wa ‘Gladiator II’ mwenye miaka 70, amefichua kuwa Novemba mwaka jana muongozaji Ryan Coogler mwenye miaka 38, alimuandikia filamu mpya, ingawa mtayarishaji Nate Moore amesisitiza Marvel haiwezi kuthibitisha kuhusika kwa Washington katika mradi huo kwa sababu studio haijawa na mazungumzo na muongozaji filamu huyo.
Akiongea na Screen Rant juu ya uwezekano wa Washington kucheza katika filamu ya ‘Black Panther 3’, Moore amesema: “Ikiwa hiyo itadhihirika, itakuwa ni kitu kizuri mno lakini hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika hgivyo ni mapema kulizungumzia hilo.
“Kwa kweli hatujafanya mazungumzo ya ubunifu na muongozaji Ryan, kwa sababu anamalizia filamu yake ya ‘Sinners’, ambayo itatoka mwaka huu filamu ambayo ni nzuri sana.
“Kwa hivyo ni mapema sana kusema, lakini ni wazi ikiwa mwigizaji wa aina ya Denzel Washington anataka kuingia, tutatafuta njia ya kufanya hivyo.” Amesema.
Washington alipokuwa akielezea miradi yake ya mwisho ingekuwaje kabla ya kustaafu kutoka Hollywood alisema kabla hajastaafu kucheza filamu huenda angeshiriki katika filamu inayofuata ya ‘Black Panther’.
Washington alikiambia kipindi cha ‘Today’ cha Australia kuwa anavutiwa kufanya kazi na walio bora zaidi, hajui atacheza filamu ngapi lakini anataka kufanya mambo ambayo hajawahi kufanya.
Nyota wa ‘The Equalizer’ alitania: “Nilicheza ‘Othello’ nikiwa na miaka 22, sasa nitacheza nikiwa na miaka 70. Baada ya hapo, ninacheza ‘Hannibal’. Baada ya hapo, nilikuwa nikizungumza na Steve McQueen kuhusu filamu nyingine.
“Baada ya hapo, Ryan Coogler ananiandikia sehemu katika ‘Black Panther’ inayofuata. Baada ya hapo, nitafanya filamu ya ‘Othello’. Baada ya hapo nitafanya ‘King Lear’. Baada ya hapo, nitastaafu.”
Filamu ya tatu ya ‘Black Panther’ itafuata kutoka kwa ‘Black Panther: Wakanda Forever’ ya mwaka 2022, na kuna uwezekano mkubwa kurejea kwa Shuri ya Letitia Wright.