Mnuka arejea kivingine Simba

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Aisha Mnuka amesema amerudi kwenye timu kuendeleza alipoishia katika kutikisa nyavu katika kila mechi kwa ajili ya kufikia malengo ya klabu hiyo.
Mnuka hakuwepo kwenye kikosi cha Simba Queens tangu kuanza kwa msimu huu na amerejea na kufanikiwa kufunga mabao mawili kati ya 11 dhidi ya Mlandizi Queens katika mchezo uliopigwa juzi Jumatano Uwanja wa KMC Complex.
Amesema hakuwepo kwenye timu kwa muda mrefu na amerejea kivingine kuendeleza alipoishia katika kufumania nyavu kama alivyomaliza msimu wa 2023/24 akiwa mfungaji bora.
“Nimefurahi kurejea kwenye kazi, nimerudi kuendeleza nilipoishia niweze kuendelea kufunga mabao, wenzangu wamenitangulia bado sijachelewa nafasi ipo naweza kumshawishi kocha kuniamini na kunipa nafasi nikafanya vizuri,” amesema.
Aisha amesema amerudi kuungana na wachezaji wenzake kuongeza nguvu katika kufikia malengo ya Simba Queens kuhakikisha wanafanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya wanawake Tanzania.