Ligi Ya Wanawake

Simba yawashika pabaya Yanga, msimu ujao vilio tu!

DAR ES SAALAM: BAADA ya kuhusishwa kuwania saini ya wachezaji wawili kutoka Yanga Princess Marry Saiki na Precious Christopher, Uongozi wa Simba Quueens umesema bado ni mapema kuliweka wazi jambo hilo kwa sababu ya idadi ya wachezaji wa kigeni ndani ya kikosi hicho.

Inadaiwa nyota hao wamemaliza mikataba yao ndani ya Yanga Princess na Simba wako kwenye mchakato wa kupata huduma zao kwa ajili ya kuimarisha kikosi kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

Akizungumza na Spotileo, Meneja wa Simba Queens, Seleman Makanya amesema licha ya dirisha la usajili kufunguliwa lakini bado hawajaanza kufanya usajili na wapo kwenye mchakato wa kuangalia aina ya wachezaji wanaotaka kusajili kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi.

Kuhusu Saiki na Precious, amesema ni wachezaji wazuri na wameonyesha kiwango kizuri msimu uliopita lakini hawawezi kuliweka wazi hilo kwa sababu ya sheria na kanuni ya idadi ya wachezaji 12 wa kigeni kuwabana.

“Saiki ni mzuri kila mmoja wetu amemuona akicheza hakuna kocha au timu itakataa huduma ya nyota huyo kama tungekuwa na nafasi kwa wachezaji wakigeni tungemchukua na kuja kuongeza nguvu ndani ya kikosi chetu,” amesema Makanya.

Amesema kwa sasa wanapitia ripoti ya benchi la ufundi linaloongozwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ na kuangalia tathimini ya msimu uliomalizika na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na kujenga Simba Queens ya ushindani mkubwa kwa ajili ya michuano ya Kimataifa.

Simba Queens ni wawakilishi wa Tanzaia katika mashindano ya Kanda ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutafuta nafasi ya kuwania kufuzu fainali za Klabu Bingwa Afrika, 2024/25.

Related Articles

Back to top button