Muziki

Mama Ongea na Mwanao yamsapoti Shusho

TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao imemuunga mkono mwimbaji wa nyimbo za injili, Christina Shusho, katika maandalizi ya tamasha la Mtoko wa Pasaka litakalofanyika Aprili 20, mwaka huu.

Tamasha hilo, linalotarajiwa kufanyika Super Dome, Dar es Salaam, limekusudiwa kuwaunganisha Watanzania kupitia nyimbo, maombi na utoaji wa misaada kwa kina mama wajawazito.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, amesema tukio hilo litakuwa maalum kwa ajili ya kuliombea taifa na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Amani tuliyopewa na Mungu lazima tuilinde kwa gharama yoyote kupitia maombi. Maombi yana nguvu kuliko mtutu wa bunduki,” amesema.

Taasisi hiyo pia imetangaza kutoa msaada kwa kina mama wajawazito katika hospitali zote za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam kuelekea kilele cha Pasaka.

Amesema kusaidia ni sehemu ya kazi yao kama taasisi yenye lengo la kuzungumzia na kugusa maisha ya Watanzania kwa vitendo.

Tamasha hilo linatarajiwa kushirikisha wasanii wa muziki kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda watakaotoa burudani, huku waimbaji wa Tanzania wakiongozwa na Shusho.

Kwa upande wake, Shusho amesema lengo kuu la tamasha hilo ni kuwaleta pamoja Watanzania na watu wa Afrika Mashariki katika amani na mshikamano.

Amesema kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Kwa Maombi Utashinda”, kauli inayoungwa mkono na wasanii wote katika kumuombea mema Rais Samia kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Related Articles

Back to top button