“Wacheza disco wanaiogopa mikopo”
DAR ES SALAAM; Mwenyekiti wa Chama cha muziki wa Disco Nchini, Hassan Bago maarufu kwa jina la Mc Cool amesema wacheza disco ndiyo wasanii pekee wenye hofu ya kuchukua mikopo ya serikali kutokana na kuporomoka kwa soko la fani yao.
Mc Cool amesema katika chama chao chenye wanachama wa fani mbalimbali baadhi yao wameshachukua mikopo ya wasanii wakiwemo “madjay” lakini wacheza disco kwao imekuwa changamoto.
Mc Cool amesema kinachofanyika kwa sasa ni kuwakutanisha wasanii hao pamoja kisha kuwajengea uwezo ili waweze kukopa na kuzalisha kupitia fani zao.
“Awali wacheza disco hawakuwa wakikidhi vigezo vya kupata mikopo lakini baada ya mabadiliko ya mikopo hiyo kwa sasa wanaweza kukopa lakini shida ni namna ya kulipa hiyo mikopo kutokana na fani yao kupungua thamani katika tasnia nzima ya sanaa,” amesema Mc Cool.
Mc Cool amesema mipango waliyoweka kwa wacheza disco wazamani na sasa ni kuwaweka kimakundi na kuwajengea uwezo wa kufanya maonyesho kimakundi ili wafanye kazi nyingi zitakazowarudisha katika umaarufu wao wa zamani.
“Kwa sasa makundi mengi ya wacheza disco yamevunjika kila mmoja anapambana mwenyewe hali ambayo inaleta ugumu kwa wasanii hao kufanikiwa kupata mkopo,” ameeleza Mc Cool.