Burudani

Lizzo akosoa unafiki wa jamii

MWANAMUZIKI mashuhuri Melissa Viviane Jefferson (Lizzo) amekosoa namna jamii inavyowatendea wanawake weusi katika tasnia ya burudani, akieleza kuwa wanashambuliwa wanapokuwa hai lakini husifiwa wanapofanikiwa au baada ya kufariki.

Kupitia mifano mbalimbali, Lizzo anaonesha jinsi mfumo wa burudani umewatendea wanawake weusi kwa dhuluma na kutopewa haki sawa kama wenzao wa kizungu.

Mmoja wa mifano yake ni msanii wa filamu na muziki, Janet Jackson, ambaye mwaka 2004 alihusishwa katika tukio la Super Bowl Halftime Show, ambapo mwimbaji Justin Timberlake alichana sehemu ya vazi lake, na kusababisha sehemu ya kifua chake kuonekana hadharani.

Tukio hilo, lililopewa jina la Nipplegate, liliathiri sana kazi ya Janet Jackson, huku Timberlake akiendelea na taaluma yake bila madhara yoyote.

Miaka 20 baadaye, muziki wa Janet unapongezwa, lakini madhila aliyopitia hayawezi kusahaulika.

Pia, Lizzo alizungumzia mkasa wa Whitney Houston, aliyekuwa na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya, lakini badala ya kusaidiwa, alifanywa kuwa mzaha. Hata hivyo, baada ya kifo chake, dunia ilianza kumheshimu. Lizzo anataja tofauti katika namna ambavyo Amy Winehouse, aliyepitia matatizo sawa, alihurumiwa zaidi na jamii kwa kisa chake cha madawa ya kulevya.

Katika historia ya burudani, Tina Turner ni mfano mwingine wa mwanamke mweusi aliyepitia manyanyaso makubwa mikononi mwa mume wake Ike Turner.

Hata hivyo, badala ya jamii kuliona hili kama ukatili wa kijinsia, lilichukuliwa kama sehemu ya burudani.

Ni baada ya mafanikio yake ndipo alipopewa heshima anayostahili.

Kwa mujibu wa Lizzo, mfumo wa burudani unawalinda wasanii wa kizungu zaidi, huku wanawake weusi wakikumbana na hukumu kali na kuchelewa kupewa heshima yao. Anaeleza kuwa mwanamke mweusi ndiye mtu asiye na ulinzi kabisa nchini Marekani.

Unahisi jamii itaendelea kuwatendea wanawake weusi kwa dharau wanapokuwa hai na kuwasifu baada ya kufariki, au mabadiliko yatafanyika?

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button