KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema wachezaji kupambana ndiyo siri kubwa ya matokeo ya ushindi inayoipata timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na SpotiLeo, kocha huyo amesema pamoja na ugumu wa ratiba wachezaji wameendelea kupambana na kupata pointi tatu ambazo zimeendelea kuiweka timu katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
“Wachezaji wanaendelea kujitoa na kuipambania jezi ya Yanga, ukweli pamoja na uchovu na ubovu wa viwanja vya mikoani lakini wameendelea kupambana na kupata ushindi jambo ambalo ndio muhimu kwetu,” amesema Kaze.
Kocha huyo amesema mpaka kufikia Novemba 31 Yanga itakuwa imecheza mechi 9 ndani ya mwezi mmoja na wiki moja.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 29 sawa na Azam baada ya michezo 11 lakini zinatofautiana kwa mabao na bado ina michezo miwili mkononi.