Howe achoshwa na tetesi

LONDON: Bosi wa New Castle United Eddie Howe amesema anachoshwa na tetesi zinazowahusisha wachezaji wa timu hiyo na klabu zingine za ndani na za nje ya Premier League.
Howe ameyasema hayo akijibu swali katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa wa raundi ya 5 ya kombe la FA dhidi ya Brighton Jumapili, swali lililouliza iwapo atakubali beki wake Mwingereza Tino Livramento ajiunge na Manchester City baada ya uwepo wa tetesi zinazomhusisha na wababe hao wa Manchester.
Amesema wanajitahidi kuunda timu imara inayoanza na saikolojia za wachezaji lakini uwepo wa tetesi za usajili wa wachezaji wake zinamvuruga si yeye tu bali wachezaji pia.
“Kwakweli inakera na kuvunja moyo, muda wote tunazungumzia wachezaji na tetesi za wao kuondoka. Tunataka kuchukua mkondo mwingine wa kuimarisha kikosi. Tunataka kufanya timu yetu iwe bora na imara kwa siku zijazo na si kupoteza wachezaji wetu, tetesi zinavuruga mipango yetu na wachezaji” amesema Howe
Siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la tetesi za mastaa kadhaa wa timu hiyo kuikacha na kutimkia kwingineko. Ukiachana na Livramento anaehusishwa na Manchester City, tetesi pia zinataja nyota wao Alexander Isak kuhitajiwa na Liverpool na Arsenal.