Guardiola : huyu Savinho mali
MANCHESTER: Kocha mkuu wa Wababe wa ligi kuu ya England Manchester city Pep Guardiola, amesema anaamini winga mpya wa klabu hiyo Savinho anauwezo wa kumudu presha na ratiba ngumu ya klabu hiyo.
Manchester City itaanza msimu mpya wa mashindano kwa mechi zenye presha kubwa na kocha Pep anaamini Savinho mwenye miaka 20 ataisaidia klabu hiyo inapopambana kufanya vizuri kwenye Ligi kuu ya England, Ligi ya mabingwa barani Ulaya na michuano mingine iliyo mbele ya klabu hiyo.
“Anafanya vizuri sana mazoezini nina uhakika anaweza kucheza kila baada ya siku 3 au 4 hili ni jambo ambalo tunalizingatia sana, ni kwa namna gani tunaweza kumtegemea mchezaji” amesema Pep
M’Brazil huyo anayemudu kucheza kama winga wa kulia na kushoto anatarajiwa kuwa kete muhimu kwenye ubao wa Guardiola wakati timu hiyo ikijipanga kutetea ubingwa wake wa ligi kuu na mashindano mengine.
Savinho alijiunga na Manchester city akitokea Girona FC alikokuwa anacheza kwa mkopo wa muda mrefu akitokea klabu ya Troyes ya Ufaransa ambako hakucheza hata mechi moja
Akiwa Girona Savinho alifunga mabao 9 katika michezo 37 aliyocheza na tayari ameshinda ngao ya jamii ya shirikisho la mpira nchini England wikiendi iliyopita akiwa na Manchester city.