Filamu

Filamu ya Nigeria yashinda tuzo ya jumla ZIFF 2026

ZANZIBAR:FILAMU ya ‘A Land Apart’ kutoka Nigeria imeibuka mshindi wa tuzo ya juu zaidi katika Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) 2026 baada ya kutangazwa kuwa Filamu Bora ya Mwaka (Best Film) kwenye hafla ya utoaji wa tuzo iliyofanyika Juni 28 mjini Zanzibar.

Filamu hiyo iliyoongozwa na Bem Pever iliiongoza Nigeria kwenye usiku wa tuzo uliohusisha washindani kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mbalimbali ya Afrika, ikiendelea kudhihirisha ukuaji wa tasnia ya filamu barani humo.

Mbali na ushindi huo, Tanzania nayo ilipata mafanikio makubwa kupitia Sultan Tamba aliyeshinda tuzo ya kwanza ya filamu iliyotengenezwa kwa kutumia Teknolojia ya Akili Bandia (AI Film) kupitia filamu ya Kilwa Kisiwani, huku tamthilia ya Noma ikitawala tuzo za mfululizo wa runinga nchini.

Katika kanda ya Afrika Mashariki, Uganda iling’ara kupitia filamu ya Small Gods iliyotwaa tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki pamoja na tuzo za waigizaji bora wa kiume na wa kike, wakati Kenya ilifanya vizuri katika kategoria za tamthilia za televisheni.

Tuzo nyingine muhimu zilikwenda kwa filamu We Are Hadza kutoka Tanzania na Marekani iliyoshinda Tuzo ya Mwenyekiti, huku filamu kutoka Ethiopia, Zambia, Ghana na Afrika Kusini nazo zikitambuliwa katika kategoria mbalimbali za ushindani.

Tamasha la mwaka huu lilifanyika kuanzia Juni 24 hadi 28 chini ya kaulimbiu “AI and the Art of Storytelling,” likiwakutanisha watengenezaji wa filamu, waigizaji, wadau wa sanaa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali kujadili mustakabali wa simulizi za Afrika na matumizi ya teknolojia katika tasnia ya filamu.

Waandaaji wa ZIFF wamesema matokeo ya mwaka huu yanaonyesha ushindani mkubwa na kuongezeka kwa ubora wa filamu za Afrika, huku tamasha hilo likiendelea kuimarisha nafasi ya Zanzibar kama kitovu cha filamu, utamaduni na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Related Articles

Back to top button