Filamu

Hanks ashangazwa na filamu zake mwenyewe

LOS ANGELES: Muigizaji nguli wa Hollywood, aliyewika kwenye filamu ya uharamia ya ‘Captain Phillips’ Tom Hanks, amesema licha ya kuwa na zaidi ya miaka 40 katika tasnia ya filamu na kushiriki katika kazi nyingi zilizotikisa duniani, anaamini ni filamu chache tu kati ya alizowahi kuigiza ndizo anaziona kuwa zimefanikiwa kwa kiwango alichokitarajia.

Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni, mshindi huyo wa tuzo mbili za Oscar alisema ubora wa filamu hauamuliwi na umaarufu wa muigizaji pekee, bali hutegemea mambo mengi ikiwemo ubora wa hadithi, maandalizi, uongozi wa mtayarishaji na jinsi kazi nzima inavyotekelezwa. Alieleza kuwa wakati mwingine filamu inaweza kuwa na waigizaji wakubwa lakini ikashindwa kufikia viwango vilivyotarajiwa.

Hanks alibainisha kuwa kutengeneza filamu bora ni mchakato mgumu unaohitaji ushirikiano wa watu wengi, akisisitiza kuwa hakuna mwigizaji anayeweza kuhakikisha mafanikio ya filamu peke yake. Kauli yake imeibua mjadala miongoni mwa mashabiki wa filamu, wengi wakijaribu kubashiri ni zipi kati ya kazi zake anazoziona kuwa bora zaidi.

Tom Hanks anahesabiwa kuwa mmoja wa waigizaji wenye mafanikio makubwa katika historia ya Hollywood, akiwa ameigiza filamu maarufu kama ‘Forrest Gump’, ‘Saving Private Ryan’, ‘Cast Away’, ‘The Green Mile’, ‘Apollo 13’ na ‘Toy Story’. Licha ya mafanikio hayo makubwa, kauli yake imeonesha kuwa hata mastaa wakubwa hujichambua na kutathmini kazi zao kwa viwango vya juu zaidi tofauti na wanavyodhaniwa.

Related Articles

Back to top button