Uwoya: Mpumzisheni Kajala, kachoka

DAR ES SALAAM: MWIGIZAJI wa filamu Tanzania, Irene Uwoya, amekerwa na kauli ya mchambuzi Ally Juma maarufu kama El Mando, baada ya kumkosoa mwigizaji Kajala Masanja kuhusu baadhi ya kauli alizotoa katika kipindi cha A List.
El Mando amedai kuwa Kajala Masanja anajishushia heshima kutokana na mambo anayoyaeleza katika kipindi hicho, kauli ambayo imeonekana kumkwaza Irene Uwoya.
Kupitia ujumbe aliouandika, Irene amemtaka El Mando kuwa makini na kauli anazotoa, akisisitiza kuwa kama kuna jambo asilolijua, ni bora kukaa kimya badala ya kutoa maoni yasiyo na msingi.
“Kitu kama hujui nyamaza, sio lazima uongee… sisi sio machizi. Hilo ni swali liliulizwa na watu wengi na mimi nilitaka liwe wazi watu wapunguze kiherehere,” aliandika Uwoya.
Irene pia amemtetea Kajala na kuwataka watu kuacha kumuandama, akisema kuwa mwigizaji huyo amechoka na anahitaji kupumzishwa.
“Mpumzisheni Kajala, kachoka jamani… mwanaume mzima unamambo ya kike,” alisema Uwoya.
Aidha, Uwoya amedai kuwa mara nyingi watu huamua kunyamaza ili kuepuka migogoro, lakini wakati mwingine kauli za watu huwalazimisha kujibu.
“Kuna muda mtu unaamua kuwa mpole ufanye yanayokuhusu, ila anatokea mtu tu anakurudisha nyuma,” ameandika.
Mwisho wa ujumbe wake, Uwoya ameonesha kuwa amefikia hatua ya kushindwa kuendelea kukaa kimya kuhusu suala hilo, akisema:
“Mungu nisamehe, ila huyu ningemwacha.”
Kauli hiyo ya Uwoya imezua mijadala huku wengine wakisema wanayoongea mengine hayaendani kwa kuwa sasa wanafamilia zao tofauti miongoni mwa mashabiki wa burudani, huku wengi wakisubiri kuona kama El Mando atajibu au suala hilo litaishia hapo.




