Kikapu

Vijana waichapa JKT, waibuka na ushindi mnono

DAR ES SALAAM: TIMU ya Vijana imeanza kuonesha makali katika Ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuichapa JKT kwa pointi 82-57 katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Don Bosco, Oyster Bay.

Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa katika robo mbili za mwanzo, ambapo timu hizo zilitoka sare ya pointi 24-24 katika robo ya kwanza na kwenda mapumzikoni zikiwa bado hazijatengana, huku ubao ukisoma 39-39.

Hata hivyo, Vijana ilibadilisha kasi katika robo ya tatu, ikitumia vyema nafasi ilizopata na kuanza kutengeneza pengo baada ya kufikisha pointi 61 dhidi ya 50 za JKT.

Katika robo ya mwisho, Vijana iliendelea kutawala mchezo na kuongeza pointi 21 huku JKT ikifanikiwa kupata saba pekee, hali iliyoiwezesha Vijana kumaliza mchezo kwa ushindi wa pointi 82-57.

Ushindi huo unaifanya Vijana kuonesha uwezo wa kupambana hadi dakika za mwisho, baada ya JKT kuonekana kuwa mpinzani mgumu katika kipindi cha kwanza kabla ya kushindwa kuhimili kasi ya wapinzani wao katika robo mbili za mwisho.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Reel Dreams iliibuka na ushindi wa pointi 63-52 dhidi ya Jeshi Stars, huku Tausi Royals ikiichapa Don Bosco Lioness 66-39.

Don Bosco Troncat yenyewe ilipata ushindi mnono wa pointi 69-38 dhidi ya Mgulani Queens katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button