Zuchu: Nilifunga siku 22 nikiwa mjamzito

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’, amefunguka kuhusu kipindi chake cha ujauzito na kueleza kuwa aliweza kutekeleza ibada ya kufunga kwa siku 22 katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani licha ya kuwa katika hali hiyo.
Kauli ya msanii huyo imeibua komenti na kuvutia hisia za mashabiki wengi katika mitandao ya kijamii, huku baadhi wakionesha kuvutiwa na uthabiti wake wa kiibada na wengine wakitaka kufahamu zaidi namna alivyoweza kuhimili kipindi hicho.
Zuchu alitoa maelezo hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii baada ya kuulizwa na mmoja wa wafuasi wake kuhusu uzoefu wake wa Ramadhani akiwa mjamzito.
Akijibu swali hilo kwa ufupi, Zuchu ameandika: “Kipindi cha mimba nilifunga siku 22.”
Kauli hiyo imezua maoni mbalimbali kutoka kwa mashabiki wake, wengi wakimpongeza kwa kujituma katika ibada na kuonyesha uvumilivu katika kipindi cha ujauzito.
Kwa sasa, Zuchu anaendelea kuwa miongoni mwa wasanii wanaofuatiliwa kwa karibu nchini na nje ya Tanzania, huku maisha yake binafsi na safari yake ya muziki vikiendelea kuvutia mashabiki wengi kwenye majukwaa mbalimbali ya kijamii.




