Mtoto wa Hamisa ahitimu darasa la saba

DAR ES SALAAM: MTOTO wa kwanza wa mwanamitindo, Hamisa Mobetto, Fantacy amehitimu elimu ya msingi, hatua iliyozua furaha kubwa kwa familia na mashabiki wake.
Katika picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Fantacy ameonekana akiwa amevalia mavazi ya mahafali sambamba na mama yake, Hamisa Mobetto, ambaye alionyesha furaha na fahari kubwa kufuatia mafanikio hayo ya mwanaye.
Hatua hiyo imepokelewa kwa pongezi nyingi kutoka kwa mashabiki na wadau mbalimbali, huku wengi wakimtakia kila la heri katika safari yake mpya ya elimu ya sekondari.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Hamisa ameeleza hisia zake za furaha na mshangao kuona jinsi muda ulivyopita haraka tangu alipokuwa akimlea Fantacy akiwa mtoto mdogo hadi kufikia hatua hiyo muhimu ya elimu.
“Kweli siku hazigandi… Baby Fantacy amemaliza Primary School! It feels like just yesterday ulikuwa mtoto wangu mdogo, na leo hii nakutazama ukifunga chapter hii na kuanza nyingine,” ameandika Hamisa.
Hamisa amesema anajivunia maendeleo ya mwanaye na namna anavyoendelea kukua kuwa binti mwenye maadili na malengo makubwa ya maisha.
“Mwanangu, Mama is beyond proud of you and the beautiful young lady you are becoming,” ameongeza.
Mbali na pongezi hizo, Hamisa amemshukuru Mungu kwa kumwezesha Fantacy kufikia hatua hiyo muhimu, akisema neema na ulinzi wa Mungu umeendelea kuwa sehemu ya safari yao.
Aidha, amemuombea mwanaye aendelee kuongozwa na Mungu, alindwe na kubarikiwa katika kila hatua ya maisha yake, huku akisisitiza kuwa kuhitimu Darasa la Saba ni mwanzo wa mafanikio makubwa yanayomsubiri siku zijazo.
“Keep shining, my baby girl. Mama will always be your biggest cheerleader. On to the next chapter!” ameandika Hamisa.
Mahafali hayo yamekuwa miongoni mwa matukio yaliyovutia hisia za mashabiki wa Hamisa Mobetto, wengi wakimpongeza Fantacy kwa hatua hiyo na kumtakia mafanikio zaidi katika masomo yake.




