
DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Elias Barnaba, ametangaza rasmi kuingia katika tasnia ya filamu baada ya kuzindua tamthilia yake mpya ya Kikulacho Season 1 kupitia kampuni yake ya High Table Film.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Barnaba amesema wengi hawafahamu kuwa safari yake ya sanaa ilianzia kwenye uigizaji kabla hajajikita kikamilifu kwenye muziki wa Bongo Fleva.
“Nilipopata tatizo la kuungua, kesho yake nilikuwa natakiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya uzinduzi wa Kikulacho, lakini kutokana na yaliyotokea nililazimika kuusogeza mbele. Leo rasmi tunazindua tamthilia hii ambayo itakuwa ikirushwa kupitia chaneli yetu ya YouTube,” amesema Barnaba.
Amesema lengo la kuanzisha mradi huo ni kuinua na kutangaza vipaji vipya vya uigizaji, kuongeza ushindani katika tasnia ya filamu, kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wasanii na wadau wa sekta hiyo, pamoja na kukuza soko la filamu nchini.
Barnaba ameongeza kuwa anaamini tamthilia hiyo itatoa fursa kwa waigizaji chipukizi kuonesha uwezo wao na kujijengea majina katika tasnia ya filamu.
Kwa upande wake, mwigizaji chipukizi Aisha Juma maarufu kama Khan, ambaye ni miongoni mwa waigizaji walioshiriki katika tamthilia hiyo, amempongeza Barnaba kwa hatua yake ya kusaidia kukuza na kuibua vipaji vipya kupitia mradi huo.
Amesema uwekezaji wa Barnaba katika filamu ni mchango mkubwa kwa tasnia hiyo, hasa kwa wasanii wanaotafuta nafasi za kuonesha uwezo wao mbele ya hadhira kubwa.




