‘Bebi’ wa Rihanna kwenda jela miaka 24?

LOS ANGELES: MWANAMUZIKI wa Pop Rihanna amefika mahakamani kwa mara ya kwanza kusikiliza mwenendo wa kesi inayoendelea ya mpenzi wake wa muda mrefu na baba mtoto wake, A$AP Rocky, anayekabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kumpiga risasi rafiki yake wa zamani, A$AP Relli, nje ya hoteli ya Los. Angeles.
A$AP Rocky, ambaye jina lake halisi ni Rakim Athelston Mayers, amekana mashitaka hayo na iwapo atapatikana na hatia, anaweza kufungwa jela miaka 24.
Kesi yake imekuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu na mashabiki, vyombo vya habari, na hata wanamtandao ambao sasa wanaelekeza mawazo yao kwenye uwepo usiotarajiwa wa Rihanna katika chumba cha mahakama wakidai kwamba huenda ikabadilisha mwenendo wa kesi hiyo.
Siku ya Jumatano, Rihanna, ambaye anaishi na watoto wawili wadogo na Rocky, aliketi kortini mbali na kamera, pembeni yake alikuwepo mama yake na dada yake.
Mwanamuziki huyo nyota wa pop na mfanyabiashara bilionea aliingizwa ndani kabla ya vyombo vya habari kuingia chumbani, akikwepa umati na kamera alipokuwa amekaa nje ya mahakama hiyo ya jiji la Los Angeles.
Uwepo wake mara moja ulizua wimbi la uvumi mtandaoni, huku wanamtandao wakigawanyika iwapo kujitokeza kwake mahakamani hapo kulikuwa ni jambo la kimkakati au onyesho la kumuunga mkono mpenzi wake.
Wengi kwenye mitandao ya kijamii walionyesha wakati wa kuwasili kwake, huku wengine wakipendekeza kuwa kuonekana kwa Rihanna kunaweza kuwa ni hatua ya kujitangaza ili kuondoa umakini katika kesi hiyo na kuhukumu yake iwe ya huruma.
Mtumiaji mmoja kwenye X aliandika kwamba ujio wa Riahanna katika mahakama hiyo utawafanya watu wote kumzungumzia yeye badala ya kujadili na kuzungumzia hukumu ya mpenzi wake.
“…Nilidhani Rihanna hatatokea hadi hukumu itakaposomwa. Walakini, ni PR nzuri. Kila mtu atazungumza kuhusu Rihanna badala ya ushuhuda wa Relli kufyatuliwa risasi…”