
DAR ES SALAAM:MKURUGENZI wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo, amewahamasisha wanafunzi wa kike nchini kujikita katika masomo ya sayansi, akisisitiza kuwa urembo haupaswi kuwa kikwazo cha kufanikiwa katika taaluma hizo.

Jokate ametoa wito huo wakati wa ziara ya kielimu iliyolenga kuhamasisha ujifunzaji wa sayansi nje ya darasa, ambapo alisisitiza umuhimu wa kubadili mfumo wa ufundishaji kwa kuzingatia zaidi mafunzo ya vitendo kuliko nadharia pekee.
Amesema mbinu ya kujifunza kwa vitendo huchangia kuongeza uelewa wa kina kwa wanafunzi, huku pia ikiwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha halisi.

“Ni muhimu kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo ili waweze kuelewa wanachofundishwa na kutumia maarifa hayo katika maisha yao ya kila siku,” amesema Jokate.
Aidha, ameeleza kuwa elimu ya vitendo huwasaidia wanafunzi kukuza ubunifu, ujuzi na uwezo wa kutatua changamoto, mambo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Kidoti Foundation imebainisha kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwawezesha vijana kufikiri kwa kina, kubuni na kuwa viongozi bora wa baadaye.
“Tunalenga kuona vijana wetu hawafaulu mitihani tu, bali pia wanakuwa wabunifu na wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii,” amesema mwakilishi wa taasisi hiyo.
Naye mwanafunzi wa sayansi, Rahma Shomari, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupanua mafunzo ya vitendo ili kuwapa wanafunzi uzoefu halisi wa kile wanachojifunza darasani, hatua itakayoongeza ufanisi wao kielimu.
Katika kuimarisha juhudi hizo, Kidoti Foundation kwa kushirikiana na Project Inspire waliandaa ziara ya kielimu kwa wanafunzi wa sayansi kutoka Shule ya Sekondari Jokate kwenda STEM Park.
Ziara hiyo iliyofanyika leo imewakutanisha takribani wanafunzi 120 kutoka Kisarawe, na kuwapa fursa ya kipekee kujifunza sayansi na teknolojia kwa vitendo, tofauti na mfumo wa kawaida wa darasani unaotegemea nadharia pekee.




