Anceloti huyooo Saudia
MADRID: MWANAHABARI Ramon Alvarez kutoka jiji la Madrid amedai kwamba meneja wa sasa wa Real Madrid, Carlo Ancelotti anaifikiria ofa aliyoipata kutoka Saudi Arabia mara tu atakapoachana na Los Blancos.
Kwa mujibu wa mwanahabari huyo Ancelotti ambaye ni Muitaliano anaripotiwa kuwa na ofa kuu mezani kutoka Saudi Arabia. Ingawa uamuzi haujafanywa bado, inaonekana kuwa vilabu vya Saudi vina nia ya kupata huduma yake kwa mradi wao wa kandanda unaokua.
Huku kukiwa na tetesi hizi, mwandishi huyo ameeleza kwamba Real Madrid wanaendelea kumtazama Xabi Alonso kama mtu sahihi wa kuchukua mikoba ya Ancelotti muda ukifika.
Alonso, ambaye amekuwa akivutia kama kocha mkuu wa Bayer Leverkusen, anasalia kuwa mtangulizi wa nafasi hiyo mara tu Ancelotti atakapoondoka.
Wazo la Alonso kuingia kwenye nafasi ya ukocha katika klabu ya Real Madrid limekuwa likijadiliwa sana kwa muda sasa, kutokana na uhusiano wake wa karibu na klabu hiyo na uwezo wake wa ukocha.
Carlo Ancelotti mwenyewe alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kwamba Real Madrid ndiyo itakuwa klabu yake ya mwisho katika kazi yake ya ukocha ngazi ya klabu.
Hata hivyo, Ancelotti ameacha wazi mlango wa kuitumikia timu ya taifa, huku tetesi zikivuma kuhusu ofa inayoweza kutolewa na timu ya taifa ya Brazil baada ya kumalizana na Real Madrid.
Ancelotti aliongeza mkataba wake na Real Madrid mnamo Novemba 2023, na kunyamazisha uvumi wa kuondoka kwake karibu hapo. Mkataba wake unatarajiwa kudumu hadi 2026, lakini maswali kuhusu mustakabali wake unaendelea kuzungumzwa na wadau wengi wa soka.