Alonso anaiwaza Bayern huyo!
KOCHA mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ujerumani, Bayer Leverkusen Xabi Alonso amesema mchezo wa ligi hiyo dhidi ya mabingwa wa kihistoria Bayern Munich utakuwa mchezo mgumu sana hasa baada ya kutazama kiwango cha wababe hao wa Bundesliga msimu huu.
Alonso amesema Bayern wameanza vizuri ligi hiyo na michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya hivyo Leverkusen wanahitaji kuwa kamili kuwakabili vigogo hao.
“Tunahitaji utendaji mzuri ili turudi nyumbani na pointi. FC Bayern wameanza vyema msimu huu, itakuwa mechi kali na ya ushindani sana kesho”.
“Tunahitaji kucheza kwa kiwango chetu cha juu zaidi, tukiwa na mpira na hata bila mpira kwa dakika 90 bila kuchoka. Bayern watakuja ‘full mkoko’ , lazima tuwe tayari kwa hilo.” amesema Alonso
Bayern wamedhamiria kurejesha makali yao chini ya kocha mpya Vincent Kompany, na tayari vigogo hao juu ya kilele cha Bundesliga kwa pointi tatu dhidi ya Leverkusen wanaoshika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo kabla ya mechi hii kubwa kwa timu hizo itakayopigwa Uwanjani wa Allianz Arena kesho Jumamosi saa moja usiku.
Bayern wameshinda mechi 4 katika 4 za Bundesliga walizocheza, wamefunga mabao 16 na wamefungwa matatu pekee. Huu ni mwanzo bora zaidi wa msimu mmoja kwa klabu kwenye historia ya Bundesliga ni Bayern hao hao waliowahi kufanya hivyo msimu 2016-17 na Stuttgart mnamo 1996-97.