Bayern yamtimua Tuchel
KLABU ya Bayern Munich itaachana na kocha wake Thomas Tuchel mwisho wa msimu kufuatia klabu hiyo kuwa na mwenendo mbaya.
Bayern imekuwa na wiki kadhaa ngumu baada ya kukandwa mabao 3-0 na vinara wa Bundesliga, Bayer Leverkusen, kupokea kichapo cha bao 1-0 toka Lazio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kipigo cha mabao 3-2 toka VfL Bochum 1848.
Klabu hiyo sasa inakabiliwa na uwezekano wa kumaliza msimu bila kombe kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2021-12 huku Leverkusen ikiwa pointi 8 zaidi ya Bayern katika msimamo wa Bundesliga.
Katika taarifa kwenye tovuti ya klabu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Jan-Christian Dreesen amesema:”Katika mazungumzo ya wazi, mazuri tumefikia uamuzi wa pande mbili kusitisha ushirikiano wetu majira yajayo ya kiangazi.”
Tuchel pia ameelezea uamuzi huo.
“Tumekubaliana kwamba tutamaliza ushirikiano wetu baada ya msimu huu. Hadi wakati huo, mimi na timu yangu ya ufundi bila shaka tutaendelea kufanya kila tunaloweza kuhakikisha tunapata mafanikio ya juu,” amesema Tuchel.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea aliyejiunga na Bayern Machi 2023 ana mkataba unaofikia tamati Juni 2025, hata hivyo timu hiyo ya Bavaria imechagua kuupunguza kwa mwaka mmoja.