Mashindano ya golfu kuanza Agosti 1 Lugalo

DAR ES SALAAM: Mashindano ya Gofu ya Vodacom Corporate Masters 2026 kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited yanatarajiwa kuanza Agosti 1, 2026 katika viwanja vya Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kukuza ushirikiano na kuleta fursa zenye tija.
Mashindano hayo yanatumika kama jukwaa kuu la udhamini wa mchezo wa golf kwa sekta ya biashara, lililobuniwa kuunganisha jumuiya ya wafanyabiashara nchini huku likiimarisha nafasi ya Vodacom katika teknolojia na huduma za mawasiliano kwa taasisi na mashirika yanayoendelea kukua katika mazingira ya uchumi wa kidijitali.
Mashindano hayo yatawakutanisha wakuu wa makampuni, wafanyabiashara, wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wapenzi wa mchezo wa golf pamoja na wateja wa Vodacom ambao watashiriki katika mfululizo wa mashindano hayo pamoja na matukio ya kujenga mitandao ya kibiashara yatakayofanyika kwenye uwanja wa Lugalo Golf Club.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi alisema mashindano hayo yanalenga kuimarisha uhusiano na jumuiya ya wafanyabiashara nchini.
“Vodacom tunaamini kuwa ukuaji endelevu wa biashara unajengwa kupitia mahusiano imara na yenye maana. Mashindano ya golf ya Vodacom Corporate Masters 2026 ni zaidi ya mashindano ya michezo, hili ni jukwaa linalowakutanisha viongozi wa biashara, wabunifu na watoa maamuzi ili kujenga uhusiano, kubadilishana mawazo na kusaka fursa mpya zitakazochangia ajenda ya Tanzania ya mageuzi ya kidijitali. Kupitia mpango huu tunaendelea kuziwezesha biashara kwa kutoa suluhisho za teknolojia zenye uhakika huku tukiwapa wateja na wadau wetu uzoefu wa kipekee,” alisema Sayi.
Katika kipindi chote cha mashindano hayo, Vodacom Business itaonesha suluhisho zake bunifu za kidijitali zinazojumuisha huduma za mawasiliano, usalama wa kidijitali pamoja na teknolojia za biashara zinazosaidia taasisi kuongeza ufanisi wa shughuli zake, kuharakisha ukuaji na kuendelea kuwa na ushindani katika dunia inayozidi kutegemea teknolojia.
Mwenyekiti wa Corporate Masters, Ken Kariuki alielezea mashindano hayo kuwa ni jukwaa la kipekee la ushirikishwaji wa makampuni linalowezesha kuongeza muonekano wa chapa, kujenga mitandao ya kibiashara, kuzalisha fursa za biashara na kuimarisha ushiriki wa wateja.

Tukio hilo la siku moja litashirikisha timu 10 za kampuni zitakazoshindania kombe la Vodacom Corporate Masters 2026, sambamba na eneo maalum la makampuni litaklokuwa na burudani, maonesho mbalimbali, maonesho ya vitu vya kale (vintage) pamoja na eneo maalum la watoto, hivyo kuweka mazingira rafiki kwa familia, kwa washiriki na wageni watakaohudhuria.
Mashindano ya golf ya Vodacom Corporate Masters yanaendelea kudhihirisha dhamira ya Vodacom Tanzania ya kujenga ushirikiano wa kuaminika na kuunga mkono mipango inayozalisha thamani ya kudumu kwa wateja, biashara na jamii.




