Mshindi wa jumla ‘Lina PG Tour’ Jumapili

DAR ES SALAAM: MSHINDI wa jumla wa michuano ya gofu ya Lina PG Tour anatarajia kupatikana Jumapili hii katika Viwanja vya Dar Gymkhana.
Mashindano hayo yalifanyika katika mikoa tofauti na sasa yanaenda kuhitimishwa ambapo mshindi wa jumla atawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai.
Miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki shindano hilo ni Isack Wanyeche amesema michuano hiyo ni fursa na furaha kwake kushiriki na anaamini kwa msaada wa Mungu atafanikiwa kwenda Dubai na kuiwakilisha Tanzania kuputia mchezo huo.
“Kama mchezaji wa gofu wa kulipwa ni heshima kushiriki katika mashindano haya kumuenzi mchezaji mwenzetu wa zamani, tunaendelea na mashindano na tunamuomba Mungu ili niendelee kufanya vizuri na kujiweka katika nafasi nzuri” amesema.
Naye Mchezaji wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Arusha, Nuru Mollel amesema kuwa amejiandaa vyema kwa mashindano hayo na anaimani ataendelea kufanya vizuri.
“Mashindano haya yameandaliwa vyema na nimekuja kwa maandalizi na nimekuja kushindana,tumefanya sehemu yetu ya kujiandaa, lakini mwishowe, tunamuachia Mungu mwenyewe, kwani yeye anajua kila kitu.” amesema.
Michuano hiyo ya gofu ya Lina PG Tour imeandaliwa na familia ya Said Nkya kwa kushirikiana na Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kwa lengo la kumuenzi mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya gofu Marehemu Lina aliyekuwa na mchango mkubwa kwenye timu na TLGU.
Lina alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania mwaka 2011 walipotwaa taji la Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Dar es Salaam.