Simba yaacha nyota saba

DAR ES SALAAM: Klabu ya Simba imeanza kufanya maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano baada ya kutangaza kuachana na wachezaji saba, wakiwemo waliokuwa wakitumika kwa mkopo katika klabu mbalimbali.
Katika orodha hiyo, wachezaji watano waliokuwa kwenye mikataba ya mkopo wamerejea kutoka kwenye timu walizokuwa wakicheza, huku Simba ikiamua kutowaendeleza katika mipango yake ya msimu ujao.
Wachezaji hao ni Omari Omari aliyekuwa akiitumikia Mashujaa FC, Joshua Mutale aliyekuwa Al-Adalah ya Saudi Arabia, Chamou Karaboue aliyekuwa TRA United, Awesu Awesu aliyekuwa Polisi Kenya pamoja na Edwin Balua aliyekuwa Al Entisar ya Saudi Arabia.
Mbali na wachezaji hao waliokuwa kwa mkopo, Simba pia imeachana na nyota wawili raia wa Guinea ambao walikuwa sehemu ya kikosi hicho, Naby Camara na mlinda mlango Moussa Camara.
Moussa Camara alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya muda mrefu yaliyomuweka nje kwa kipindi kirefu, hali iliyomfanya kushindwa kutoa mchango unaotarajiwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Hatua hiyo imekuja wakati Simba ikiendelea na mipango ya kujenga kikosi kipya chenye ushindani kuelekea msimu wa 2026/27, ambapo inatarajiwa kufanya usajili wa wachezaji wapya katika maeneo mbalimbali ya timu.




