Twiga Stars kujipima na Nigeria, Mali Wafcon

DAR ES SALAAM: Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, Bakari Shime amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) yanaendelea vizuri, huku akieleza kuwa mechi za kirafiki zitakazochezwa Morocco zitasaidia kufanya tathmini ya mwisho kabla ya kuanza kwa mashindano.
Shime amesema Twiga Stars inatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki ikiwemo dhidi ya Nigeria Julai 19 na mwingine Julai 22 na dhidi ya Ghana au Mali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wao wa kwanza wa mashindano dhidi ya Afrika Kusini Julai 26.
Amesema michezo hiyo itakuwa nafasi muhimu kwa benchi la ufundi kupima uwezo wa wachezaji na kufanya marekebisho katika maeneo mbalimbali kabla ya kuingia kwenye vita ya WAFCON.
“Malengo ya michezo hii ni kuona timu yetu inafanya vizuri, kuongeza nguvu na kurekebisha mambo muhimu kabla ya kuanza kwa mashindano,” amesema Shime.
Kocha huyo amesema katika mashindano yaliyopita walikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo majeraha ya wachezaji muhimu, uchovu wa kikosi na muda mfupi wa maandalizi, lakini safari hii wamefanya kazi kubwa kuhakikisha wanakuwa katika hali nzuri.
“Tulikuwa na changamoto kubwa ya majeruhi kwenye timu yetu, hasa wachezaji tegemezi, lakini safari hii tumeweza kuyasimamia vizuri na kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kiafya na kimwili,” amesema.
Shime amesema baada ya kuweka kambi Karatu kwa takribani wiki tatu, wamefanyia kazi maeneo muhimu ya mchezo ikiwemo namna ya kujilinda, kujenga mashambulizi, kushambulia pamoja na kuongeza utimamu wa mwili.
Aidha, Shime amesema mabadiliko yaliyofanywa na CAF kwenye WAFCON, ikiwemo kuongeza idadi ya wachezaji kutoka 23 hadi 26 na kuongeza muda wa mapumziko kati ya mechi, yatasaidia timu kusimamia vizuri ratiba ya mashindano.




