Ahmed Ally: Kwa Kagoma mtasubiri sana

UONGOZI wa Simba umetupa dongo kwa wapinzani wao wanaohitaji huduma ya kiungo wao, Yusuph Kagoma kwamba wasubiri miaka 10 ijayo.Kauli hiyo ya Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameitoa baada ya Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, kumtaka mchezaji huyo kuomba msamaha kwa alichowafanyia ili wamruhusu kuichezea klabu yake ya sasa, Simba.
Yanga imepeleka shauri kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji juu ya mchezaji huyo kuwa alichukua pesa zao na kusaini mkataba, lakini baadaye wakasikia amesaini tena kwenye Klabu ya Simba.
Hata hivyo, Kamwe alidai ili wamwachie, wanataka mchezaji huyo aombe radhi, la sivyo watamhesabu kama ni mchezaji ambaye amesaini pande mbili.
Ahmed Ally ameliambia Spotileo kuwa kuna klabu inampenda sana Kagoma kila wakilala wanamuota.
Alisema roho zinawauma kumkosa kiungo huyo na wanamtaka kwenda kwao wawe na subira kwa sababu nyota huyo yupo Simba akiwa na miaka 23.
“Kwa uwezo wa Mungu atakaa Simba miaka 10 mbele akifikisha miaka 33 au 35 ndio ataenda kwao wanaomtaka, Yaani mfumo ni ule ule kama walivyomsubiri Mzambia kwa miaka 7.
Vilevile walivyomsubiri namba 20 kwa miaka 15 kwa Kagoma ni hivyo hivyo kwa sababu ni mali ya Simba,” amesema Ahmed.