Muziki

Mwimbaji wa Reggae Fantan Mojah afariki dunia

JAMAICA: Tasnia ya muziki wa reggae duniani imepata pigo kufuatia kifo cha mwanamuziki maarufu wa Jamaica, Fantan Mojah, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49, zikiwa zimebaki wiki tatu afikishe miaka 50.

Kifo chake kimewaacha mashabiki na wanamuziki wengi katika majonzi, wakimkumbuka kwa nyimbo zake zenye ujumbe wa matumaini, imani ya Rastafari na haki za jamii.

Fantan Mojah alifariki Jana jioni katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha West Indies (UHWI) jijini Kingston, Jamaica, baada ya kupata matatizo ya moyo yaliyosababisha hali yake kuzorota ghafla.

Kwa mujibu wa wakala wake wa maonesho, Vertex, msanii huyo alianza kuugua siku chache baada ya kurejea kutoka Marekani, ambapo afya yake ilianza kudhoofika kwa kasi kabla ya kulazwa hospitalini. Alieleza kuwa usiku wa mwisho kabla ya kufariki, Mojah alianza kutapika damu na baadaye alifariki akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Kabla ya kifo chake, Fantan Mojah alikuwa akijiandaa kushiriki Tamasha la Reggae Jam Festival nchini Ujerumani baada ya kupata visa ya Schengen kwa ajili ya ziara hiyo. Hata hivyo, ndoto hiyo haikuweza kutimia kutokana na hali yake ya afya. Katika siku zake za mwisho alikuwa akiishi na marafiki zake mjini Portmore, Jamaica, huku akishindwa kufanya shughuli nzito kutokana na udhaifu wa mwili.

Mwimbaji huyo alikuwa akipambana na matatizo makubwa ya afya kwa miaka kadhaa. Mwaka 2024 alilazwa hospitalini nchini Martinique baada ya kupata matatizo ya kupumua na maumivu ya kifua, ambapo ilielezwa kuwa moyo wake ulikuwa ukifanya kazi kwa takribani asilimia 15 pekee. Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka 2025 alionekana kuimarika na kurejea jukwaani kwa kufanya ziara za muziki barani Ulaya.

Fantan Mojah, ambaye anaripotiwa kuacha watoto wasiopungua watano, atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizobeba ujumbe wa kiroho, mapenzi, amani na mshikamano. Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika muziki wa reggae, huku mashabiki na wasanii kutoka sehemu mbalimbali duniani wakimuenzi kama mmoja wa sauti muhimu zilizotetea falsafa ya Rastafari kupitia muziki.

Related Articles

Back to top button