Ahmed Ally anyoosha maelezo ishu ya Awesu Awesu
DAR ES SALAAM:MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amefafanua juu ya sintofahamu iliyoibuka juu ya usajili wa kiungo wao mpya kutoka KMC FC, Awesu Awesu.
Kuna taarifa iliibuka kutoka kwa viongozi wa KMC FC baada ya Simba kumtambulisha Awesu ikisema kuwa klabu hiyo mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam haijafuata taratibu za usajili na kwenda mbali kuwa kiungo huyo bado ni mchezaji wa KMC.
Ahmed amesema viongozi wa Simba wako makini katika usajili wao na kuhoji ni kwa nini sajili ya ndani ziwe na kelele na kuonekana Simba wanafanya uhuni?, wamefuata taratibu zote za usajili kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2024/25.
“Kwa nini sajili za ndani ndio ziwe na kelele, kwa nini isiwe usajili wa nyota wa kigeni tumemsajili Debora Fernandes, Augustine Okejepha , Joshua Mutale na wengine lakini hakuna hizo kele za kuwa Simba ni wahuni.
Simba hawafanyi uhuni, bali tunaofanya nao kazi ndio wanaleta uhuni, tuweza kufuata taratibu kwenye kufanya usajili wa mchezaji kutoka Ivory Coast au Ghana tushindwe kujua utaratibu wa nyota mzawa,” amesema Ahmed.
Amewashusha presha ya mashabiki wa klabu hiyo kuwa wachezaji wote ambao wamewasajili wamefuata taratibu zote za usajili na suala la Awesu limekamilika kisheria na taratibu zote za usajili.
Kuhusu suala la Aubin Kramo, Ahmed amesema nyota huyo hayupo kwenye mipango ya Simba kwa msimu wa 2024/25 kwa sababu ya tathimini ya kimatibabu na kiufundi kuona hataweza kuwezana na presha ya mashabiki wa Simba kwa msimu mpya.
“Kramo ametoka katika majeraha makubwa na kutokana na msimu huu utakuwa wa presha kubwa tumeona bora kumtafutia timu aende kwa mkopo au kuachana naye. Maana hataweza presha za mashabiki wanachokihitaji ni ubingwa tu,” amesema Ahmed.