Nyumbani

Mmemsikia Aziz Ki?

DAR ES SALAAM: KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, amesema kuna mambo mazuri yanakuja msimu huu wa 2024/25 katika mashindano yaliyopo mbele yao.

Amesema timu yao msimu huu ni bora kuliko msimu uliopita na kuahidi kufanya makubwa zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania wakiyataka makombe yote watakayoshiriki.

Aziz Ki ambaye ni MVP wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, ameyasema hayo siku chache baada ya Yanga kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 mbele ya wanalambalamba Azam FC katika Fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa dimba la Benjamin Mkapa.

Mfungaji huyo bora wa msimu uliopita ambaye pia alichangia bao moja katika ushindi huo mbele ya Azam FC amesema, anaamini msimu huu mashabiki wa Yanga watapata furaha kubwa kutokana na aina ya kikosi walichonacho.

“Ilikuwa ni ngumu sana kushinda mbele ya Simba na Azam FC lakini tumefanikiwa kupata matokeo. Tupo vizuri ninaamini tutafanya makubwa zaidi kuanzia Ligi Kuu na hata michuano ya Kimataifa,” alisema Aziz Ki.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Prince Dube, aliyesajiliwa kutoka kwa wanalambalamba hao, mengine mawili walinzi wao wakijifunga huku bao la nne likiwekwa wavuni na straika matata wa kikosi hicho Clement Mzize.

Kwa sasa wanajangwani hao wanajiandaa kwa mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wakata miwa wa Kagera Sugar, ugenini mwishoni mwa wiki hii wakipewa nafasi kubwa kupata matokeo mazuri.

Related Articles

Back to top button