Nyumba ya Lamine Yamal yanusurika kuvamiwa na majambazi

BARCELONA: Nyota wa Hispania na klabu ya Barcelona, Lamine Yamal, amekumbwa na mshtuko baada ya nyumba yake iliyopo Esplugues de Llobregat, nje kidogo ya jiji la Barcelona, kulengwa na majambazi waliotaka kuvamia nyumba hiyo saa chache baada ya kuisaidia Hispania kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa na kutinga fainali ya Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa polisi wa Catalonia pamoja na vyombo vya habari vya Hispania, watu wawili waliokuwa wamejifunika nyuso walinaswa na kamera za ulinzi wakijaribu kuruka ukuta wa nyumba hiyo, lakini walinzi binafsi waliokuwa wakilinda eneo hilo waligundua tukio hilo mapema na kuchukua tahadhari iliyowalazimu wahalifu hao kutoroka kabla ya polisi kufika eneo la tukio. Uchunguzi umeanza huku picha za CCTV zikitumika kuwabaini wahusika.

Wakati tukio hilo likitokea, Yamal hakuwepo nyumbani kwani alikuwa nchini Marekani na kikosi cha Hispania baada ya kung’ara katika ushindi dhidi ya Ufaransa, ambapo alitoa mchango mkubwa uliowasaidia mabingwa hao wa Ulaya kufuzu kucheza fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 na kwenye fainali watachuana na mabingwa watetezi wa kombe hilo Argentina.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa wanasoka maarufu barani Ulaya, huku nyumba za mastaa kadhaa zikilengwa na wahalifu wakati wachezaji wanapokuwa safarini au wanashiriki mechi muhimu.
Licha ya tukio hilo, Yamal anatarajiwa kuendelea na maandalizi ya mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia huku Kitengo cha Polisi Hispania kikiendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika.




