Ligi Daraja La Kwanza

Tamasha la ZIFF 2026 lazinduliwa kiaina

ZANZIBAR:MSIMU wa 29 wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026) umezinduliwa kwa shamrashamra kubwa na maonesho ya kipekee ya utamaduni katika Ukumbi wa Wangazija wa Wakfu, huku ukiwakutanisha wasanii, watayarishaji wa filamu, wanadiplomasia na wadau wa sanaa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Uzinduzi huo uliopambwa na burudani za asili za Kizanzibari, gwaride la tamasha na maonesho mbalimbali ya kisanii, uliashiria rasmi kuanza kwa siku tano za shughuli za filamu, majadiliano ya kitaaluma, mafunzo na maonesho ya kazi za wabunifu kutoka Afrika na mataifa ya Ukanda wa Nchi za Dhow.

Akizungumza katika hafla hiyo, viongozi wa tamasha hilo walieleza kuwa ZIFF 2026 imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza filamu za Kiafrika na kuunganisha tamaduni mbalimbali kupitia sanaa, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikitoa nafasi kwa mijadala kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI) katika usimulizi wa hadithi na utengenezaji wa filamu.

Mbali na maonesho ya filamu, tamasha hilo pia limeandaa mijadala ya kitaaluma, warsha za ubunifu, maonesho ya sinema za wazi pamoja na matukio ya kitamaduni yanayolenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika sekta ya sanaa na ubunifu.

ZIFF, ambayo imekuwa ikifanyika Zanzibar tangu mwaka 1997, inaendelea kutambulika kama moja ya matamasha makubwa ya filamu na utamaduni katika Afrika Mashariki, huku ikichangia kuitangaza Zanzibar kimataifa kama kitovu cha utalii wa sanaa, filamu na urithi wa kitamaduni.

Related Articles

Back to top button