Ayra Starr amfuata Idris Elba kwenye filamu

LAGOS: MKALI wa muziki kutoka Nigeria, Ayra Starr, na muigizaji nguli Richard Mofe-Damijo, ni miongoni mwa wasanii walioongezwa kwenye filamu inayotokana na riwaya ya Tomi Adeyemi, Children of Blood & Bone, ambayo inaendelea kuandaliwa huku matangazo ya awali kuhusu filamu hiyo yakipokelewa vyema mitandaoni.
Mastaa wengine walioungana katika mradi huo ni Pamilerin Ayodeji, Shamz Garuba, na mchezaji wa mpira wa kikapu mwenye asili ya Marekani na Nigeria, Temi Fagbenle, mzaliwa wa London.
Kwa upande wake, Starr, ambaye ni maarufu kwa kipaji chake katika muziki, anajiunga na Mofe-Damijo, mkongwe wa tasnia ya filamu nchini Nigeria anayefahamika kwa uhusika wake katika filamu mbalimbali, ikiwemo The Black Book.
Filamu hiyo itaongozwa na Thuso Mbedu, nyota wa The Woman King, ambaye atachukua nafasi ya mhusika mkuu mwenye nguvu, Zélie. Tosin Cole, anayejulikana kwa Supacell, atacheza nafasi ya Tzain, kaka mkubwa wa Zélie.
Amandla Stenberg na Damson Idris wanatazamiwa kuigiza kama Princess Amari na Prince Inan, huku mwigizaji maarufu wa Uingereza na Nigeria, Chiwetel Ejiofor, akiingia kwenye nafasi ya Mfalme Saran.
Ili kuongeza mvuto wa filamu hiyo, waigizaji wengine wakubwa waliopo kwenye mradi huo ni pamoja na Viola Davis, Idris Elba, Cynthia Erivo, Lashana Lynch, na mshindi wa Tuzo ya Academy, Regina King, ambao watashiriki katika uwasilishaji wa mhusika Malkia Nehanda.
Filamu hiyo, ambayo bado inaendelea kutayarishwa, imepangwa kutolewa mapema mwaka 2027 na inatarajiwa kufanya vizuri katika soko la filamu duniani.