Tuchel: Bellingham apigania nafasi ya kwanza

ENGLAND: KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel amesema kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham anapaswa kupigania nafasi yake ili kuingia katika kikosi cha kwanza cha England katika Kombe la Dunia.
Tuchel amesema kikosi chake cha sasa kina ushindani mkubwa sana, kiasi kwamba hata wachezaji wenye majina makubwa wanapaswa kuonesha ubora wa ziada ili kupata nafasi ya kuanza.
Ameeleza kuwa Bellingham ni miongoni mwa wachezaji anaowachukulia kama sehemu ya kikosi cha kwanza, lakini ushindani ndani ya timu ni mkubwa sana kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wenye kiwango sawa.
Kocha huyo amemtaja pia kiungo wa Aston Villa, Morgan Rogers, kama mchezaji aliyekuwa na nafasi kubwa katika michezo ya hivi karibuni, huku akicheza mara nyingi chini ya uongozi wake.
Bellingham amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara tangu Tuchel alipochukua uongozi wa England mwaka 2025, hali iliyosababisha mjadala mkubwa kuhusu nafasi yake ndani ya timu hiyos.




