De la Fuente: Tumerudisha roho ya Hispania ya 2010

TEXAS: Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente, amesema kikosi chake kimefanikiwa kufufua ari na umoja uliokifanya taifa hilo kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 baada ya kuifunga Ufaransa mabao 2-0 na kutinga fainali ya michuano hiyo.
Akizungumza baada ya ushindi huo mjini Arlington, Texas, De la Fuente amesema wachezaji wake walionesha nidhamu, mshikamano na vipaji vya hali ya juu dhidi ya Ufaransa, ambayo ilikuwa imefunga mabao 16 kabla ya hatua ya nusu fainali.
“Ujumbe wetu ulikuwa rahisi, tulikuwa tunacheza dhidi ya moja ya timu bora duniani, lakini wao pia walikuwa wanacheza dhidi ya timu bora duniani,” amesema kocha huyo.
Alieleza kuwa mafanikio ya Hispania yametokana na umoja wa kikosi, unyenyekevu na kila mmoja kuweka maslahi ya timu mbele kuliko ya binafsi.
“Tumerejesha roho ya mwaka 2010. Nimeona furaha kubwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na taifa zima likiwa nyuma yetu. Hata wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza walibaki kufanya mazoezi baada ya mechi, jambo linaloonesha tabia ya kikosi hiki,” amesema.
De la Fuente amesema mafanikio hayo si ya bahati, bali ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu uliojengwa kwa malengo ya kuifikisha Hispania katika kiwango bora wakati muhimu wa mashindano.
Ushindi huo umeifanya Hispania kufikisha michezo 37 mfululizo bila kupoteza, ikiisawazisha rekodi ya Italia, huku ikiwa imebakiza ushindi mmoja pekee kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia yake.
Kuhusu mpinzani wa fainali, De la Fuente amesema angependa kukutana na Argentina kutokana na urafiki wake na kocha Lionel Scaloni, lakini akasisitiza kuwa pia ana heshima kubwa kwa England na anaamini nusu fainali yao ni mechi yenye ubora wa fainali.
“Siamini kwamba fainali zipo kwa ajili ya kushindwa au kushinda pekee. Zipo ili zifurahie, na kilichobaki kinaweza kuwa zawadi tamu zaidi ya safari yetu,” amesema.




